エピソード

  • Mungu Akifungua Mlango, Atakukuta Uko Tayari?
    2026/09/04

    🎙️ Leo kwenye Neno la Leo

    Leo kupitia 1 Samweli 16:18 tunaendelea na simulizi ya Daudi. Jana tulimwona akipakwa mafuta lakini bado hakwenda moja kwa moja kuwa mfalme. Leo tunasikia mtu akimwelezea kwa Sauli: Daudi anajua kupiga kinubi, ni shujaa, ana busara katika kusema na zaidi ya yote, Bwana yu pamoja naye.

    Jambo la kuvutia ni kwamba sifa hizi hazikuanza kujengwa siku ambayo nafasi ya kwenda ikulu ilifunguka. Daudi alikuwa ameanza kujiandaa wakati hakuna aliyekuwa akimtazama.

    Alijifunza kupiga kinubi bila kujua kwamba siku moja muziki huo ungemfungulia mlango wa ikulu. Alijifunza kuwa mwaminifu akichunga kondoo bila kujua kwamba ujasiri aliokuwa akiujenga huko malishoni ungehitajika katika hatua kubwa zaidi za maisha yake.

    Fursa ilipofika, maandalizi yalikuwa yameanza zamani.

    Nasi mara nyingi tunamwomba Mungu atufungulie milango. Tunaomba kazi, biashara ikue, huduma ipanuke, tupate cheo au nafasi kubwa zaidi. Lakini pamoja na kuomba mlango ufunguke, kuna swali jingine tunalopaswa kujiuliza: Mlango ukifunguka leo, je, niko tayari?

    Usisubiri nafasi ndipo uanze kujenga uwezo. Usisubiri watu wakutambue ndipo uanze kujenga tabia. Jenga leo kile ambacho kesho yako itahitaji. Tumia vizuri kipindi ambacho hakuna anayekuona kwa sababu huenda Mungu anakitumia kukuandaa kwa nafasi ambayo bado hujaiona.

    Lakini kati ya sifa zote za Daudi, Biblia inataja moja ambayo ni kubwa kuliko zote: “Bwana yu pamoja naye.” Tunaweza kujenga ujuzi, uzoefu na uwezo lakini maandalizi yetu makubwa zaidi ni kujifunza kutembea pamoja na Mungu.

    Kwa hiyo usiombe tu, “Bwana, nifungulie mlango.” Omba pia, “Bwana, nitengeneze ili mlango utakapofunguka, niwe tayari.”

    Karibu tusikilize, tutafakari na kujifunza pamoja. 🙏📖✨

    続きを読む 一部表示
    33 分
  • Ruhusu Mungu Akutengeneze.
    2026/09/03

    🎙️ Leo kwenye Neno la Leo

    Leo kupitia 1 Samweli 16:13 tunaendelea na simulizi ya Daudi. Jana tulimwacha malishoni, mahali ambapo watu hawakumfikiria lakini Mungu alikuwa amemwona. Leo anaitwa nyumbani na Mungu anamwambia Samweli, “Ondoka, umtie mafuta, maana huyu ndiye.” Daudi anapakwa mafuta katikati ya ndugu zake na Roho wa Bwana anakuja juu yake.

    Lakini jambo la kushangaza ni hili: Daudi alipakwa mafuta kuwa mfalme lakini hakwenda moja kwa moja kukalia kiti cha enzi.

    Alikuwa amechaguliwa lakini bado alikuwa na safari. Kulikuwa na tofauti kati ya kusudi alilopewa na utayari wa kulibeba.

    Nasi tunaweza kufanya kosa la kutaka kila kitu kitokee mara tu tunapoanza kuona kusudi la Mungu katika maisha yetu. Tunapata ndoto, maono, kipawa au nafasi fulani na tunataka jukwaa mara moja. Lakini Mungu anaweza kukuita leo na bado akatumia muda kukufundisha, kukukomaza na kuandaa tabia yako kwa kile anachotaka kukukabidhi kesho.

    Usikimbilie jukwaa kwa sababu tu umeona kusudi. Ruhusu Mungu akutengeneze.

    Daudi alipakwa mafuta kabla taifa halijamtambua. Mungu alikuwa ameona ndani yake kile ambacho wengine bado hawajakiona. Kwa hiyo kama watu bado hawaoni kile Mungu anaweka ndani yako, usiwe na haraka ya kujithibitisha. Endelea kuwa mwaminifu katika hatua uliyo nayo sasa.

    Swali si tu, “Je, Mungu amenichagua?” Swali jingine muhimu ni, “Je, ninamruhusu Mungu aniandae kwa kile alichonichagulia?”

    Kwa sababu wakati wako utakapofika, hutahitaji tu nafasi. Utahitaji uwezo na tabia ya kubeba kile ambacho Mungu amekukabidhi.

    Karibu tusikilize, tutafakari na kujifunza pamoja. 🙏📖✨

    続きを読む 一部表示
    19 分
  • Usidharau Mahali Ulipo Sasa!
    2026/09/02

    🎙️ Leo kwenye Neno la Leo

    Leo kupitia 1 Samweli 16:11 tunaendelea na safari tuliyoanza jana. Samweli amefika nyumbani kwa Yese kumpaka mafuta mfalme mpya wa Israeli. Wana wa Yese wanapita mbele yake mmoja baada ya mwingine lakini Mungu hamchagui hata mmoja. Hatimaye Samweli anauliza, “Je, hawa ndio wanao wote?”

    Ndipo tunagundua kwamba kuna mmoja ambaye hata hakuitwa. Daudi yuko malishoni akichunga kondoo.

    Fikiria hilo. Mfalme ajaye wa Israeli yuko shambani wakati mkutano unaohusu maisha yake unaendelea nyumbani. Hakualikwa, hakutajwa mwanzo na hakuna aliyedhani kwamba ndiye ambaye Mungu alikuwa akimtafuta. Lakini kutokualikwa na watu hakumaanishi alikuwa amesahaulika na Mungu.

    Na huenda hilo ndilo Neno la leo kwa mtu fulani. Unaweza kujisikia kama uko “malishoni” wakati wengine wako mbele ya Samweli. Wengine wanapandishwa vyeo, wanatambuliwa, wanapewa nafasi na wanaonekana kusonga mbele huku wewe ukiendelea kufanya kazi ileile ambayo hakuna anayeshangilia.

    Usidharau mahali ulipo sasa.

    Daudi hakujua kwamba mikono iliyokuwa ikilinda kondoo siku moja ingelinda taifa. Hakujua kwamba mazingira yale ya kawaida yalikuwa sehemu ya maandalizi ya Mungu kwa maisha yake. Mahali ambapo hakuna anayekuona panaweza kuwa mahali ambapo Mungu anakutengeneza.

    Kwa hiyo usidharau kazi ndogo. Usidharau majukumu yasiyoonekana. Usidharau kipindi ambacho hakuna anayekutambua. Endelea kuwa mwaminifu. Mungu anaweza kutumia kile unachofanya leo kukuandaa kwa kile ambacho bado hujakiona.

    Na kumbuka hili: Unaweza kuwa umefichika kwa watu lakini hujafichika kwa Mungu. Watu wanaweza kusahau kukuita lakini Mungu hajakusahau.

    Karibu tusikilize, tutafakari na kujifunza pamoja. 🙏📖✨

    続きを読む 一部表示
    37 分
  • Mungu Haangalii Sura, Anaangalia Moyo Wako!
    2026/09/01

    🎙️ Leo kwenye Neno la Leo

    Leo kupitia 1 Samweli 16:7 tunaanza mwezi mpya na hatua mpya katika simulizi ya 1 Samweli. Agosti tuliimaliza na Sauli, mtu aliyeanza vizuri lakini ambaye hatua kwa hatua alianza kuweka maamuzi yake mbele ya utiifu kwa Mungu. Sasa Samweli ametumwa nyumbani kwa Yese kumtafuta mfalme mwingine.

    Anapomwona Eliabu, Samweli anavutiwa na kile kinachoonekana kwa macho. Anaonekana kama mtu anayefaa kuwa mfalme. Lakini Mungu anamfundisha jambo ambalo litakuwa msingi wa safari yetu na Daudi: mwanadamu huangalia sura ya nje lakini Bwana huangalia moyo.

    Na hapo ndipo tunapoanzia Septemba: moyoni.

    Tunaishi katika dunia inayotufundisha kujenga kile watu wanaweza kuona. Muonekano, elimu, cheo, fedha, mafanikio, followers na namna tunavyoonekana mbele za wengine. Lakini Mungu anaona mahali ambapo hakuna mwanadamu anayeweza kuona kikamilifu. Anaona nia zetu, tamaa zetu, sababu zinazotusukuma kufanya tunayofanya na tabia yetu wakati hakuna anayetuangalia.

    Hii ndiyo tofauti tutakayoanza kuiona kati ya Sauli na Daudi. Siyo kwamba Daudi alikuwa mkamilifu. Tutakuja kuona makosa yake pia. Lakini Mungu alikuwa akitafuta moyo unaoweza kumrudia, kumsikiliza na kutengenezwa naye.

    Kwa hiyo tunapoanza mwezi huu, labda kabla hatujamwomba Mungu abadilishe kazi yetu, biashara yetu, mahusiano yetu au mazingira yetu, tuanze na ombi la ndani zaidi: “Bwana, tengeneza moyo wangu.”

    Na swali letu la kwanza la Septemba liwe hili:

    Mungu akiangalia moyo wangu leo, anaona nini?

    Kwa sababu watu wanaweza kuvutiwa na kile kilicho nje lakini Mungu huanzia ndani.

    Karibu tusikilize, tutafakari na kujifunza pamoja. 🙏📖✨

    続きを読む 一部表示
    30 分
  • Kuanza Vizuri Haitoshi, Linda Imani Yako Mpaka Mwisho!
    2026/08/31

    🎙️ Leo kwenye Neno la Leo

    Leo kupitia 1 Samweli 15:35 tunafunga safari yetu ya mwezi wa Agosti katika sehemu yenye huzuni. Samweli anamwombolezea Sauli na tunaona huzuni iliyotokana na mwelekeo ambao maisha ya Sauli yalikuwa yamechukua. Ni mwisho mzito lakini wenye somo muhimu sana: si muhimu tu kuanza vizuri, ni muhimu kuendelea kutembea na Mungu.

    Tulianza mwezi huu na Hana, mwanamke aliyefika mbele za Mungu akiwa na maumivu, akamimina moyo wake kwake na kujifunza kusubiri. Tukaona Mungu akimjibu na kupitia Samweli tukajifunza kusikiliza sauti ya Mungu, kumtii, kukumbuka Ebenezeri zetu na kuendelea kuwa waaminifu.

    Kisha tukamwona Sauli. Alianza akiwa mtu aliyepewa nafasi kubwa na Mungu. Lakini hatua kwa hatua presha, hofu ya watu na utiifu wa masharti vikaanza kuathiri safari yake. Na tunapofika mwisho wa sura ya 15, tunakutana na matokeo ya mwelekeo huo.

    Hili linaweza kuwa somo kubwa tunalobeba tunapofunga Agosti: ushindi wa jana hauondoi hitaji la utiifu wa leo. Hatutosheki kusema tulianza vizuri, tuliwahi kuwa karibu na Mungu au Mungu aliwahi kututumia. Kila siku tunahitaji kuendelea kumruhusu Mungu atengeneze mioyo yetu.

    Paulo alipofika mwisho wa safari yake alisema, “Mwendo nimeumaliza, imani nimeilinda.” Hilo liwe ombi letu pia. Si kwamba hatutakosea njiani bali tunapoanguka tunamrudia Mungu na kuendelea kutembea naye.

    Tunapofunga mwezi huu, swali letu liwe: Si tu nilianzaje, bali ninaendeleaje? Je, moyo wangu bado unamsikiliza Mungu? Je, bado niko tayari kumtii?

    Tusiombe tu Mungu atusaidie kuanza vizuri. Tumwombe atupe neema ya kubaki waaminifu na kumaliza vizuri.

    Karibu tusikilize, tutafakari na kujifunza pamoja. 🙏📖✨

    続きを読む 一部表示
    25 分
  • Utii ni Bora Kuliko Dhabihu!
    2026/08/30

    🎙️ Leo kwenye Neno la Leo

    Leo kupitia 1 Samweli 15:22–23 tunafika katika moja ya nyakati muhimu sana katika maisha ya Sauli. Mungu alikuwa amempa agizo lakini Sauli hakulitekeleza kikamilifu. Alipoulizwa kwa nini, akatoa sababu iliyosikika ya kiroho: baadhi ya vitu vilihifadhiwa ili vitolewe sadaka kwa Bwana. Ndipo Samweli akasema maneno ambayo yameendelea kutukumbusha mpaka leo: “Kutii ni bora kuliko dhabihu.”

    Tatizo la Sauli halikuwa kwamba hakumtii Mungu kabisa. Alitii sehemu ya agizo na akaacha sehemu ambayo haikumfaa. Kisha akajaribu kutumia jambo la kidini kuhalalisha kile ambacho Mungu hakumwagiza.

    Na hapo ndipo Neno la leo linapotufikia sisi pia. Je, inawezekana nasi tukawa tunamtii Mungu kwa masharti yetu? Tunaweza kwenda kanisani, kuomba, kutoa sadaka, kusoma Neno na kuwahudumia wengine lakini wakati huohuo tukawa tunapuuza jambo ambalo tunajua Mungu anatutaka tulirekebishe. Ibada haiwezi kuwa mbadala wa utiifu.

    Swali la leo si tu, “Je, ninamtii Mungu?” Bali ni: “Je, ninamtii Mungu hata pale mapenzi yake yanapopingana na yale ninayotaka?” Kwa sababu utiifu wa kweli hauchagui maagizo yanayotufaa na kuacha yale yanayotugharimu.

    Mungu hatutafuti tu kuwa watu wanaofanya mambo yanayoonekana ya kiroho. Anataka mioyo inayoweza kusema, “Bwana, hata kama ni vigumu, nitakutii.”

    Karibu tusikilize, tutafakari na kujifunza pamoja. 🙏📖✨

    続きを読む 一部表示
    23 分
  • Mungu Hahitaji Wengi Ili Kufanya Makubwa!
    2026/08/29

    🎙️ Leo kwenye Neno la Leo

    Leo kupitia 1 Samweli 14:6 tunamwona Yonathani akiwa na mchukua silaha wake wakikabiliana na mazingira ambayo kwa macho ya kibinadamu yanaonekana hayawezekani. Ni watu wawili tu dhidi ya jeshi kubwa la Wafilisti. Lakini Yonathani anatamka ukweli wenye nguvu: “Hakuna kinachoweza kumzuia Bwana kuokoa kwa wengi au kwa wachache.”

    Neno la leo linatukumbusha kwamba mara nyingi tunapima uwezekano wa mafanikio kwa kile tulichonacho. Tunaangalia fedha zetu, watu tulio nao, uzoefu wetu, elimu yetu au ukubwa wa nafasi tuliyopewa na kusema, “Hiki hakitoshi.” Lakini kile ambacho hakitoshi mikononi mwetu kinaweza kuwa zaidi ya kutosha kinapowekwa mikononi mwa Mungu.

    Yonathani hakukataa ukweli kwamba walikuwa wachache. Alichokataa ni kuufanya udogo wao kuwa kipimo cha uwezo wa Mungu. Hilo ndilo somo letu leo. Imani si kujifanya kwamba hatuna mapungufu. Imani ni kuyatambua mapungufu yetu lakini kukataa kuamini kwamba yanamweka Mungu mipaka.

    Je, kuna jambo ambalo umeacha kulijaribu kwa sababu unaona ulicho nacho ni kidogo? Kumbuka: Mungu hahitaji uwe na kila kitu ili aanze kufanya jambo. Anaweza kutumia kidogo ulichonacho kutimiza jambo kubwa kwa utukufu wake.

    Karibu tusikilize, tutafakari na kujifunza pamoja. 🙏📖✨

    続きを読む 一部表示
    20 分
  • Je, Unaweza Kumsubiri Mungu Wakati Kila Kitu Kinaenda Vibaya?
    2026/08/28

    🎙️ Leo kwenye Neno la Leo

    Leo kupitia 1 Samweli 13:13–14 tunaanza kuona ufa mkubwa katika uongozi wa Sauli. Wafilisti wanatishia Israeli, watu wanaanza kutawanyika na Samweli haonekani kufika kwa wakati ambao Sauli alitarajia. Akiwa chini ya presha, Sauli anaamua kuchukua hatua mwenyewe. Tatizo halikuwa kwamba hakufanya chochote. Tatizo ni kwamba alifanya jambo ambalo Mungu hakumwagiza kwa sababu hakuweza kusubiri.

    Neno la leo linatukumbusha kwamba wakati mwingine presha ndiyo hufunua kina cha utiifu wetu. Ni rahisi kusubiri wakati kila kitu kiko sawa. Lakini je, tunaweza kuendelea kumtii Mungu wakati muda unaonekana kuisha, watu wanaondoka na mazingira yanatuambia, “Fanya kitu sasa!”?

    Hapa tunakumbushwa pia safari ya Hana tuliyoiona mwanzoni mwa 1 Samweli. Hana alijifunza kusubiri mpaka wakati wa Mungu ufike. Sauli anatuonyesha upande mwingine: kile kinachoweza kutokea tunaposhindwa kusubiri. Njia ya haraka si lazima iwe njia sahihi na kuchelewa tunakokiona si ruhusa ya kutangulia mbele ya Mungu.

    Je, kuna jambo katika maisha yako ambalo presha inakusukuma kuliamua haraka? Kabla hujachukua hatua, jiulize: Ninaongozwa na Mungu au ninaongozwa na hofu kwamba muda wangu unaisha? Wakati mwingine tendo kubwa zaidi la imani si kufanya kitu haraka bali kuwa na subira ya kusubiri na kubaki katika utiifu.

    Karibu tusikilize, tutafakari na kujifunza pamoja. 🙏📖✨

    続きを読む 一部表示
    26 分